Wafanyabiashara mpoooo!!!!!!

KARIBU TUKUKUTANISHE NA WANUNUZI UPIGE HELA! Ewe mfanyabiashara, mjasiliamali, msanii, mbunifu, mkulima karibun uoneshe na kuuza bidhaa zako kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka kuanzia 13-20 Julai 2019 kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea. Mbali na wanunuzi, tamasha litakukutanisha na makampuni mbalimbali. Kwa maelezo/ushiriki tucheki: 0689 086435 au http://www.majimajiselebuka.com

MajimajiSelebukaFestival #TamashaLaMajimaji2019

FAINALI YA MDAHALO KWA SHULE ZA SEKONDARI TAMASHA LA MAJIMAJI SELEBUKA 2018

imageedit_1_3062518179NA MWANDISHI WETU, SONGEA

SHULE ya Sekondari Londoni iliyopo Lizaboni mjini Songea Mkoa wa Ruvuma imeibuka vinara wa jumla katika mashindano ya Mdahalo ‘Debating’ yaliyoandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Songea-Mississippi (SOMI), kupitia tamasha la Majimaji Selebuka.

Shindano hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Songea mkoani Ruvuma ambako Mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA), na Benki ya NMB waliokuwa wadhamini.

Mada shindaniwa ilikuwa ni faida na hasara za ulipaji kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki ‘EFD’s’.

Katika kipengele hicho cha Ushindi wa Jumla ‘Best School Over All’, Londoni ilifuatiwa na Sekondari ya Ruhuwiko huku nafasi ya tatu ikishikwa na Songea Boys.

Kipengele cha Uwasilishaji Bora ‘Best Presentation School’ Songea Girls waliibuka washindi wakifuatiwa na Peramiho Girls huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Daora kutoka jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi Bora ‘Top 5 Best Presenters’ waliopenya ni Elda Simwamba kutoka Peramiho Girls ambaye alikuwa kinara, Yusto Mwaiginsya kutoka Sekondari ya De Paul, Faines Msola wa Songea Girls, Nasma Ally wa Daora na Christandus Mhagama kutoka Luwawasi Sekondari.

Pia kulikuwa na shindano la uchoraji vibonzo, ambako Oscar Ngonzi wa Sekondari ya Pehisco aliibuka mshindi akifuatiwa na Mwanaidi Mbunde wa Maposeni huku nafasi ya tatu ikienda kwa Sharifa Makarani wa Sekondari ya Londoni.

Washindi walizawadiwa zawadi mbalimbali ikiwamo tuzo, fedha taslimu, vifaa vya kitaaluma na kimichezo, kufunguliwa akaunti benki ya NMB na kuwekewa kianzio.

Aidha,  walimu waliofanikisha shule zao kufanya vizuri walikabidhiwa zawadi za fedha taslimu.

Akizungumza kabla ya Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo, aliwapongeza waandaaji na washiriki, kwani wanatoa mchango mkubwa katika kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa jamii.

“Waandaaji wangeweza kulenga kitu kingine, lakini wameamua kuandaa mada hii, tunawashukuru kwani wanajenga walipa kodi wajao…Wengi wetu tumelikuta hili ukubwani ndio maana unaona kuna ukakasi kwa baadhi ya watu katika kulipa kodi,” alisema na kuongeza.

Lakini jamii ikijengewa uelewa na kuelewa faida za ulipaji kodi itasaidia serikali katika ukusanyaji wa kodi na kufanikisha kuendesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Kwa upande wake Mgeni rasmi, Dk. Ndumbaro, mbali na kuwapongeza washiriki na kuwataka kuwa mabalozi wema katika kutoa elimu juu ya faida ya ulipaji kodi.

Dk. Ndumbaro, alibainisha kuwa tofauti kubwa ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea na ufanyaji kazi na ulipaji kodi.

“Nchi haiwezi kuendelea bila kufanya kazi, kwenye wanafunzi kazi kubwa ni kusoma kwa bidii na pia kushiriki stadi za mikono…Wenzetu nchi zilizoendelea wanachapa kazi sana na kulipa kodi zinazojenga nchi na nyingine tunazoenda kuomba misaada, lakini sisi ni wavivu na visingizio vingi katika kazi na kutoona umuhimu wa kulipa kodi,” alisema Dk. Ndumbaro.

Aidha, alisisitiza kuwa ulipaji kodi ni uchumi hivyo asiyelipa kodi ni adui wa maendeleo na anapaswa kupigwa vita.

Dk. Ndumbaro ambauye pia ni Mkurugenzi mwenza wa SOMI, aliwapongeza TRA na NMB na kwamba tamasha la mwakani litakalofanyika kuanzia Julai 13-21 kwa upande wa mdahalo mada itaendelea kuwa ulipaji kodi katika maeneo mengine zaidi ya mashine za kielektroniki iliyokuwepo mwaka huu.

WATANZANIA WANG’ARA MAJIMAJI SELEBUKA MARATHON

Na Mwandishi Wetu

TAMASHA la Majimaji Selebuka 2018 limekata utepe jana mjini hapa kwa mbio za Marathon huku ikishuhudiwa Nestory Hudu kutoka Singida akiwatoa nishai Wakenya.

Hudu aliibuka kidedea katika mbio za Kilomita 42 kwa Wanaume akitumia saa 2:21:25 akifuatiwa na John Leonard wa Arusha saa 2.22:09 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Simon Lelei kutoka Kenya saa 2.22:54.

Kwa upande wa Wanawake Kilomita 42 mshindi aliibuka Purity Biwott wa Kenya alishinda akitumia saa 2.43:59 akifuatiwa na  Dorcus Chesang pia wa Kenya aliyetumia saa 2.45:21 huku nafasi ya tatu ikienda kwa  Angel John wa Arusha aliyetumia saa 2:53.44.

Kwa upande wa Kilomita 21 Wanaume  Pascal Sarwat wa Manyara alishinda akitumia saa 1.11:58 akifuatiwa na  Samson Lyimo wa Songea saa 1.12:13 huku Mohamed Dulle wa JWTZ Ruvuma akikamata nafasi ya tatu akitumia saa 1:12:34 wakati kwa Wanawake Tabitha Kibeth wa Kenya alishinda akitumia saa 1.21: 34 kutoka Kenya akifuatiwa na Violeth Adam wa Njombe akitumia 1.22:43 huku nafasi ya tatu ikikosa mshindi

Kwa upande wa Walemavu Kilomita 21 mshindi aliibukaDavid Mabula akifuatiwa na John Stephano huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Mathias Jollo wote kutoka Dar es Salaam.

Pia kulikuwa na Mbio za Mita 800 kwa wanafunzi ambao walitia for a kwa mwitikio mkubwa na vipaji, kwa wavulana Felix Ndunguru alishinda akitumia dakika 2.46:00 akifuatiwa na Bashiru Ngonyani dakika 2:49.2 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Franco Justine aliyetumia dakika 2:52.

Kwa wasichana Magreth Thadei alitumia 2:58.53 akifuatiwa na Hadija Mohamed dakika 2:58.55 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Maisha Mwera dakika 2:59.03.

Mbali na washindi kujizolea zawadi ya fedha taslimu na medali, pia walipata ofa ya kutembelea Mbamba Bay Beach.

Majimaji Selebuka Festival imeandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Songea-Mississippi (SO-MI), kwa kushirikiana na Tanzania Mwandi chini ya udhamini wa Bakhresa Group of Companies, Premier Bet, BIT Tech Ltd/Meridian Bet.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Riadha Mkoa wa Ruvuma, Christian Matembo, alielezea kufurahishwa na muitikio wa washiriki mwaka huu ambao walifikia zaidi ya 200 walijitokeza huku watoto wakitia for a.

Baada yam bio, tamasha linaendelea leo kwa maonyesho ya wajasiriamali, mashindano ya ngoma za asili.

Ruvuma wazidi kuneemeka na Majimaji Selebuka

thumb_DSC_5754_1024

Na Mwandishi Wetu, Songea

UWEPO wa tamasha la kila mwaka mkoani Ruvuma la Majimaji Selebuka, imegeuka kuwa neema kubwa ndani ya mkoa huo kutokana na fursa mbalimbali kwa wananchi, hiyo ni baada ya serikali ya Poland kupitia kaimu balozi wake hapa nchini, Ewelina Lubieniecka kuwathibitishia wananchi uwepo wa mkakati wa kujengwa kwa ghala kubwa la mahindi mkoani humo lenye uwezo wa kuhifadhi mahindi zaidi ya tani elfu 40 litakalokubwa kubwa kulinganisha na maghala mengine hapa nchini

Bi Ewelina amesema hatua hiyo ni mpango wa serikali ya Poland na Tanzania ambapo wanatarajia kujenga jumla ya maghala matano hapa nchini hata hivyo ghala kuu litakuwa mkoani Ruvuma kwa kile alichoeleza ni kutokana na heshima waliyopewa na waratibu wa Tamasha la Majimaji Selebuka kama mgeni rasmi katika mdahalo wa wafanyabiashara uliyofanyika Julai 16, 2018.

Aidha kupitia mdahalo huo uliyofanyika kwenye ukumbi wa manispaa Songea ulilenga kujadili changamoto na kibiashara pia kutoa elimu ya uhifadhi wa mazao ya chakula na kibiashara kwa njia ya kisasa kwa wananchi wa Ruvuma, balozi huyo alialikwa na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Dr Damas Ndumbaro ambaye pia ni mwanzilishi mwenza wa Majimaji Selebuka.

Pamoja na mengine, mdahalo huo pia ulijikita kutoa elimu kwa wakulima njia ya uhifadhi bora wa mazao kwa njia ya kisasa kupitia maghala hayo yatakayojengwa na kuwasihi wakulima kuachana na uhifadhi kimazoea ambayo yamekuwa na madhara na hasara.

“Tanzania imepewa kipaumbele zaidi katika kuleta maendeleo kwa hapa Afrika, tupo (Poland) tunajenga hospitali, shule lakini pia kwa sasa tumeweka mkazo zaidi kwenye sekta ya kilimo hasa korosho na mazao mengine ya kibiashara.

“Kwa heshima ya Majimaji Selebuka na Mbunge Dr Ndumbaro ambaye anaonyesha juhudi kwa kuzungumza na ubalozi wa Poland kutaka kuleta wataalamu wa kilimo kutoka Poland, ghala la Ruvuma ndilo litakuwa ghala kuu na kubwa zaidi na litabeba tani zaidi ya 40,000,” alisema Kaimu Balozi Ewelina.

Maghala mengine yanatarajiwa kujengwa maeneo ya Shinyanga, Makambako pamoja na Mbozi, lakini yenyewe yatakuwa na uwezo wa uhifadhi wa tani 20,000.

Mbali na ubalozi huo, mdahalo huo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme ambaye alipata fursa ya kujibu maswali ya wananchi yaliyoelekezwa kwa serikali kuhusu mikakati ya kumsaidia mkulima ili aweze kunufaika na kilimo, hata hivyo aliwahakikishia wakulima waliongozwa na mwenyekiti wao mkoa, Tito Mbilinyi kuwa tayari wamefanikisha kuingiza matreka ya kisasa yatakayomsaidia mkulima kuachana na kilimo cha mkono.

Aidha Mndeme alitoa changamoto kuu inayokwamisha maendeleo ya sekta ya kilimo mkoani kwake kuwa ni wananchi kuendelea kuhifadhi kwa njia ya mifuko pamoja na kutia dawa za wadudu ambayo wakati mwingine dawa hiyo imekuwa ikiwadhuru.

“Tatizo letu bado tunahifadhi mazao ‘locally’, tunategemea kutunza nafaka zetu kwa madawa hivyo kuongeza magonjwa, ndiyo maana Mhe. Mbunge ameliona tatizo hilo na kutuletea wataalamu wa uhifadhi wa kisasa zaidi, hii itaokoa sana sekta hii,” alisema Mndeme.

Tamasha la Majimaji lilikata utepe Julai 14 na litahitimishwa Julai 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea ambalo pamoja na fursa za kibiashara pia linajikita kuinua vipaji vya michezo mkoani humo kama vile riadha, mbio za baiskeli, soka, sambamba na kuinua sekta za Utalii wa Ndani, Utamaduni wa Asili pamoja na elimu kupitia mashindano ya mdahalo kwa shule za sekondari.