Kikundi cha Ngoma ya Mganda kutoka Luhagala wakionyesha manjonjo katika kusaka mkwanja wa ubingwa
Washindi wa mashindano ya Ngoma za Asili kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka linaloendelea kufanyika mjini Songea katika viwanja vya Majimaji.
Na Mwandishi Wetu
KASI ya awamu ya tano chini ya Amri Jeshi Mkuu, Dkt John Pombe Magufuli imezidi kutikisa kila kona ya nchi, huku wananchi wakizidi kummwagia sifa kede kede.
Ndivyo ilivyokuwa kwenye tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka linaloendelea kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, ambako vikundi karibu vyote vya ushiriki jumbe zao zilihusu ubora, ufanisi wa awamu yake ya utawala.
Mashindano hayo ambayo yalidumu kwa siku mbili na fainali kufanyika Jumanne, Julai 25, mwaka huu yalishuhudiwa Kikundi cha Mganda kutoka Luhagala kikiubuka na ushindi na kujinyakulia kombe na kitita cha laki nne.
Aidha kwa kiasi kikubwa kikundi hicho kilibebwa zaidi na ujumbe wa nyimbo zao katika kuisifia serikali ya Tanzania awamu ya tano kama vile inavyopambana na ufisadi, wala rushwa, kutokomeza biashara ya madawa ya kulevya huku wakimalizia na kibonzo cha HAPA KAZI TU
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Kikundi cha Ngoma cha Ruvuma Championi, kinachoundwa na watoto wanahosiwa kutofikisha miaka 18 ambako waliwakonga nyonyo watazamani kwa umahiri wao wa kucheza ngoma za asili. Waliondoka na kombe na fedha taslim laki tatu huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Kikundi cha Ngoma cha Kioda kinachoundwa na kina mama kutoka Luhagala. Walipewa kombe na fedha taslim laki mbili.
Mbali na fainali hizo, pia maonyesho ya ujasiriamali na utalii wa ndani ni baadhi ya shughuli zinazoendelea. Tamasha hilo litahitimishwa Julai 30, mwaka huu kwa mashindano ya mbio za baiskeli 100km kutoka Wilaya ya Mbinga mpaka Songea.
Kikundi cha Ngoma cha Ruvuma Championi, kikifanya yake jukwaani kwenye fainali ya ngoma za asili katika Tamasha la Majimaji Selebuka linaloendelea kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, Ruvuma.
Ruvuma champion pamoja na waandaaji wa tamasha la Majimaji Selebuka
Haikuwa rahisi kupatikana kwa bingwa wa ngoma za asili, kiasi cha kuwalazimu waratibu wa tamasha kutumia siku mbili ili kujidhirisha na aliyestahili kupewa zawadi ya mshindi. Kwanza ni kutokana na wingi wa vikundi, tofauti na msimu wake wa kwanza ambako vilishiriki vikundi tano,safari hii vilichuana vikundi 12pili ni ushindani wa hali ya juu.
Mazingira haya yalipelekea kutengwa kwa siku mbili, ambapo siku ya kwanza ilikuwa ya mchujo katika mfumo wa makundi ambapo kulikuwa na makundi matatu; Ngoma ya Mganda, Kioda na Ngoma ya Mchanganyiko. Kila kundi lilitoa bingwa kabla ya kukutanishwa siku iliyofuatia.
Kikundi cha Jakaya Sanaa Ngoma ya Lizombe kutoka Lizaboni, kiliibuka bingwa katika fainali ya mabingwa kwa kuviangusha Kilagano Ngoma ya Mganda (wa pili) na Boma Jaribu Ngoma ya Kioda iliyoshika nafasi ya tatu.
Washindi wote walitunukiwa zawadi ya kombe, cheti seti za fulana na fedha taslim, lakini katika kujali zaidi fani ya watu, Asasi ya Somi na Kampuni ya Mwandi Tanzania wakaingia mkataba wa kimasoko na bingwa, Jakaya Sanaa kuwatafutia masoko pamoja na kuwapa ofa ya kurekodi nyimbo zake kwenye kamera za kisasa za Azam TV ambao pia walikuwa bega kwa bega mwanzo mpaka mwisho wa tamasha na baadhi ya matukio yakirushwa mubashara ‘live’ ikiwemo fainali hiyo.
Siyo hilo tu, Somi na washirika wake katika kujali kazi zao, bado walimwaga zawadi kwenye hatua ya mchujo wa kusaka bingwa ambapo kulitolewa zawadi kwa washindi watatu kwa kila kategoria. Kinara alipewa laki tatu, mshindi wa pili laki mbili na laki moja ilikwenda kwa mshindi wa tatu.