TAMASHA LA MAJIMAJI SELEBUKA 2018 MAMBO NI MOTO

Tamasha la Majimaji Selebuka 2018 limekuja kivingine kabisa kwani kuna fursa kedekede zimeongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Kwa mwaka huu 2018 tamasha litafanyika kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 21 Julai mwaka 2018 katika uwanja wa Majimaji uliopo Songea mjini.

Majimaji Selebuka 2018 itakuwa na mambo yafuatayo;

  1. Maonyesho ya biashara na ujasiliamali
  2. Riadha
  3. Utalii wa ndani
  4. Mashinadano ya ngoma za asili
  5. Midahalo katika Shule za Sekondari
  6. Mbio za baiskeli
  7. Majimaji Selebuka Jukwaa la Wafanyabiashara
  8. Mpira wa miguu

Tamasha hili ni la kipekee kabisa katika mkoa wa Ruvuma kwani linatoa fursa kwa kila mtu bila kuchagua.

Ili uweze kushiriki unatakiwa kujisajili kwa kujaza fomu zinazopatikana kwenye tovuti yetu.

Kumbuka vigezo na masharti kuzingatiwa.

 

 

Mbio za walemavu zageuka gumzo kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka Mjini Songea.

Na Mwandishi Wetu, Songea

(3)
Mshindi wa pili kwenye mbio za walemavu katika tamasha la Majimaji Selebuka, John Stephano zilizofanyika tarehe 23 Julai 2017 mjini Songea kwenye viwanja vya Majimaji.

Hamasa kwenye tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka inazidi kupaa juu, hii ni kutokana na mwitikio chanya unaozidi kujionesha mwaka hadi mwaka, na mwaka huu mbio za walemavu ‘paralympic’ za 21km ndiyo imekuwa gumzo.

Ushiriki wao umetajwa kama chagizo kubwa la watazamaji kurundikana kwenye Uwanja wa Majimaji ambako hakuna kiingilio huku wengi wakionekana kuwapa hamasa tangu mwanzo wa mbio mpaka wanakabidhiwa tuzo, wengi wakiwapongeza kwa ujasili wao wa kuvuta pumzi kwa kilomita 21.

Katika mchuano huo wa kuwania kitita cha laki nne kwa bingwa, Jumapili Julai 23, kitita hicho kilitwaliwa na Shukuru Halfan aliyetumia muda wa dakika 18:13, nafasi ya pili ikichukuliwa na John Stephano aliyetumia muda wa  1:56:32 na kupewa laki tatu na mshindi wa tatu alikuwa Mathias Jolo kwa muda wa 2:08:39 na kuondoka na laki mbili.

Aidha katika jumla ya orodha ya washiriki wa mbio hizo, Halfan alishika nafasi tisa akiwapiku wengi wasio na ulemavu licha ya yeye akiwa na ulemavu wa mkono mmoja. Stephano ana upungufu wa mikono yote wakati Jolo ni mlemavu wa mguu.

Katika mahojiano maalum, Halfan amesema: “Kuna dhana ya walemavu kutojiamini katika kujaribu jambo, lakini kupitia tamasha hili nawashauri wenzangu wawe na moyo wa uthubutu na kujiamini kama wanaweza kazi yoyote sawa na wasio na ulemavu. Angalia, nimeshika nafasi ya tisa katika jumla ya washiriki 15, jiulize nimewapiku wazima wangapi?”

 

Diwani wa mwendokasi Selebuka 2016 huyu hapa

1-2

DALILI za mapema kuwa Tamasha la Majimaji Selebuka litagubikwa na vituko, burudani na vioja vya kutosha zilianza kujionyesha mapema wakati wa uzinduzi wake, mwaka 2015.

Katika msimu wake wa kwanza, tamasha hilo linalofanyika kila mwaka kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji mjini Songea, baadhi ya vioja ni ushiriki wa mama na mwanae katika mbio fupi za Km 5, Bibian Abdallah aliyekuwa kwenye kinyang’anyiro na mwanaye Shakira Abdallah pamoja na kile cha Askari wa Usalama babarani, Thomas kujitosa kwenye mbio za baiskeli Km 50, ingawa aliangukia pua.

Mwaka huu pia kulikowa na raha yake. Pamoja na kwamba wote hao hawakushiriki safari hii, lakini bado hawakuondoa ladha ya tamasha na kivutio cha kipekee kilikuwa cha diwani wa viti maalum wa Kata ya Matalawe, Judith Mbogoro ambaye aliwachachafya wanawake wenzake katika mbio za Km 5.

Mheshimiwa huyo ambaye kidogo umri umekwenda, miaka 38, kulinganisha na rundo la washiriki wengine, wengi wao wakiwa wastani wa miaka kati ya 20-27, kabla ya mbio, walimchukulia poa wakiamini asingeweza kukikimbia, lakini ajabu aliwatupilia mbali kwelikweli.

Yeye alitumia muda wa dakika 27: 28 akifuatiwa na Fatuma Ching’ang’a aliyetumia dakika 28:46, yaani unazungumzia muda wa dakika moja na sekunde 44! Utaona ni jinsi gani mwanasiasa huyo alivyo wa ‘mwendokasi’ haswa.

Judith, mbali na ushiriki wake kwenye riadha, pia alikuwa bega kwa bega tangu siku ya ufunguzi mpaka kufungwa kwa tamasha ambapo pia alikuwa mmoja wa majaji wakuu katika kinyang’anyiro cha Ngoma za Asili, achilia mbali kazi ya ushehereshahi (U-MC).   

Dar- Bulani ilifanikiwa kufanya mahojiano naye ambapo alifunguka siri ya mafanikio hayo. “Kwanza nipongeze waratibu wa tamasha lenyewe, hii ni moja ya sehemu muhimu katika kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo nchini.

“Kama kiongozi serikalini, hakika nimeguswa kwa kiasi kikubwa kuona wapo baadhi ya watu wanajali vipawa vya Watanzania wenzao. Naamini zipo sekta mbalimbali zitanufaika na tamasha hilo, ‘especially’ uwepo wa Azam TV.

“Kuhusu tuzo yangu, binafsi mimi ni mtu wa mazoezi. Nimejiwekea ratiba ya kufanya mazoezi kila siku kukimbia zaidi ya kilomita tatu. Nauzunguka Uwanja wa Majimaji (unaotumiwa na timu ya Majimaji) mara tano na kuchukua ‘session’ nyingine ya mazoezi. Ndiyo maana haikuwa shida sana kukimbia.

“Pili sinywi pombe, mambo ya starehe kwangu ‘no’, hivyo pamoja na uzee wangu, miaka 38, nimewachachafya watoto wadogo, najua walikuwa wakinibeza lakini watakuwa wamejifunza kutoka kwangu jinsi ya kujitunza ili uwe na afya bora,” anasema.

Msimu wa tatu wa tamasha hilo limepangwa kuwa kati ya Julai 23 hadi Julai 30 mwaka 2017.