Mtu Kwao Forum

mtu-kwao-watoto

Jukwaa ‘forum’ la Mtu Kwao lilikuwa moja ya shughuli zilizokuwepo katika tamasha hilo. Jukwaa hilo lililoendeshwa na balozi wa Majimaji Selebuka, Nathan Mpangala ambaye ni mchora vibonzo maarufu hapa nchini.

Tageti ya jukwaa hilo ilikuwa ni kuibua vipaji vya vipya katika sanaa ya uchoraji kwa watoto wadogo pamoja na kutoa elimu ya uchoraji vibonzo kwa kila mmoja aliyefika kwenye tamasha lenyewe.

Kama kawaida, zawadi zilitolewa kwa washindi watatu, lakini mshindi wa kwanza, Halfan Fred Mwinuka mbali na zawadi pia alipata ofa ya kusoma bure elimu yake ya sekondari mwakani katika Shule ya Sekondari ya Daora iliyopo jijini Dar es Salaam. Mwinuka alipata zali hilo akiwa anamalizia masomo yake ya darasa la saba katika Shule ya Msingi, Namtumbo, Ruvuma.

Mratibu wa jukwaa hilo, Mpangala anasema: “Kama dhumuni la tamasha lenyewe, bado tuliamini mbali na shughuli nyingine, pia tunaweza kuinua vipaji vya uchoraji hasa kuanzia ngazi za chini kabisa. Ndiyo maana tukaanzisha forum hii ambayo mwaka jana haikuwepo.

“Bahati nzuri kulikuwa na mwitikio mkubwa kwa watoto wengi (zaidi ya 30) lakini naamini mwakani itakuwa ni zaidi ya hapa.”

Maonyesho ya ujasiriamali

img_0736

Katika kumuinua mkulima na mwananchi wa kipato cha chini, SO-MI na Tanzania Mwandi waliamua kutoa nafasi ya shughuli za kijamii kama mazao na bidhaa zizalishwazo ndani na nje ya Tanzania kama sehemu ya kujitangaza kimasoko pamoja na kuuza bidhaa zenyewe.

Tofauti na mwaka jana ambako vilijitokeza vikundi 10, mwaka huu vilishiriki jumla ya vikundi 22, picha iliyoashiria kukubalika kwa tamasha hilo.

Mbali na maonyesho na mauzo ya bidhaa hizo, pia walipata kujitangaza kupitia Kituo cha Azam TV kwa mahojiano mbalimbali na huku siku ya kuhitimishwa wakihojiwa mubashara (live).

Haikuwa kazi ndogo kupatikana kwa washindi watatu, lakini kama kanuni za michuano, ilikuwa ni lazima wapatikane ambapo Chuo Huria (Open University of Tanzania) ambao tangu mwanzo hadi kufungwa kwa tamasha walikuwepo wakitoa msaada na ushauri wa kisheria bure kabisa. Yeyote aliyekuwa na tatizo la kisheria aliweza kusaidiwa kwa nguvu zote. Juhudi hizi ziliwapa tiketi ya kuwa washindi wa tatu, huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Kikundi cha Masista wa Chipole kutoka Mtakatifu Benedict ambao walikuwa na bidhaa za mvinyo aina mbalimbali, rozari, soseji, mishumaa mikubwa kwa midogo na vitu vingine vingi. Kikubwa kilichowabeba ni ubora wa bidhaa zao ambazo zote huzalishwa na wao wenyewe (hakuna mkono wa mwanaume).

Aidha, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mradi wa Lishe Bora wa COUNSENUTH ambao walikuwa wakitoa elimu juu ya lishe bora na vyakula sahihi kwa watoto na wajawazito. Pia walikuwa wakitoa elemu ya afya na usafi kwa ujumla. Washindi wote walitunukiwa vyeti, medali, kombe pamoja na fedha taslim.

Mashindano ya baiskeli Kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka 2016.

img_1414

Funga kazi ilikuwa ni mtifuano mkali wa kusaka washindi watatu katika kinyang’anyiro cha mbio za baiskeli, mbio zilizogawanywa katika kategori mbili; fupi za Kilomita 50 kutoka Jimbo la Peramiho mpaka Jimbo la Songea Mjini na Kilomita 95 kutoka wilaya ya Mbinga mpaka Wilaya ya Songea.

Kwenye mbio za Km 50, Halfan Omary aliibuka kidedea akifuatiwa na Mzea Hamisi wakati nafasi ya tatu ilikwenda kwa Titus Mlowe.

Kwenye kinyang’anyiro cha mbio ndefu, Km 95 ambazo mbali na kuwania zawadi za nono, pia washindi watatu wangejipatia nafasi ya kwenda nchini Rwanda kwa ajili ya mafunzo ya siku 10 ya kimataifa ya mchezo huo, kwa nia ya kuwaendeleza.

Salum Miraji ndiye alikuwa kinara wao kwa kutumia muda wa saa 3:10:07 akifuatiwa na Allen Nyanginywa aliyetumia muda wa saa 3:12:48 wakati Ipyana Mbogole akishika nafasi ya tatu akimaliza ndani ya muda wa saa 3:14:07.

Wote hawa walipata fursa ya kushiriki mafunzo nchini Rwanda achilia mbali tuzo za vyeti, fedha na medali walizotunukiwa kutokana na nafasi walizoshika.

Tofauti na wenzake, Miraji alitunukiwa tuzo maalam ya hisani yenye picha ya baiskeli.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo, Reinafrida Rwezaura amebainisha kuwa, badala ya kuwapeleka Rwanda, wameamua kuangalia mbali zaidi ambapo sasa watakwenda Afrika Kusini.

“Kuna mambo hayakwenda sawa katika safari ya Rwanda kwa upande wao, kwamba kwa msimu huu wamefuta ratiba ya mashindano hayo (baiskeli), lakini kama waratibu tumeaona tuwapeleke mbali zaidi na sasa watatakiwa kwenda Sauz (Afrika Kusini).

Diwani wa mwendokasi Selebuka 2016 huyu hapa

1-2

DALILI za mapema kuwa Tamasha la Majimaji Selebuka litagubikwa na vituko, burudani na vioja vya kutosha zilianza kujionyesha mapema wakati wa uzinduzi wake, mwaka 2015.

Katika msimu wake wa kwanza, tamasha hilo linalofanyika kila mwaka kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji mjini Songea, baadhi ya vioja ni ushiriki wa mama na mwanae katika mbio fupi za Km 5, Bibian Abdallah aliyekuwa kwenye kinyang’anyiro na mwanaye Shakira Abdallah pamoja na kile cha Askari wa Usalama babarani, Thomas kujitosa kwenye mbio za baiskeli Km 50, ingawa aliangukia pua.

Mwaka huu pia kulikowa na raha yake. Pamoja na kwamba wote hao hawakushiriki safari hii, lakini bado hawakuondoa ladha ya tamasha na kivutio cha kipekee kilikuwa cha diwani wa viti maalum wa Kata ya Matalawe, Judith Mbogoro ambaye aliwachachafya wanawake wenzake katika mbio za Km 5.

Mheshimiwa huyo ambaye kidogo umri umekwenda, miaka 38, kulinganisha na rundo la washiriki wengine, wengi wao wakiwa wastani wa miaka kati ya 20-27, kabla ya mbio, walimchukulia poa wakiamini asingeweza kukikimbia, lakini ajabu aliwatupilia mbali kwelikweli.

Yeye alitumia muda wa dakika 27: 28 akifuatiwa na Fatuma Ching’ang’a aliyetumia dakika 28:46, yaani unazungumzia muda wa dakika moja na sekunde 44! Utaona ni jinsi gani mwanasiasa huyo alivyo wa ‘mwendokasi’ haswa.

Judith, mbali na ushiriki wake kwenye riadha, pia alikuwa bega kwa bega tangu siku ya ufunguzi mpaka kufungwa kwa tamasha ambapo pia alikuwa mmoja wa majaji wakuu katika kinyang’anyiro cha Ngoma za Asili, achilia mbali kazi ya ushehereshahi (U-MC).   

Dar- Bulani ilifanikiwa kufanya mahojiano naye ambapo alifunguka siri ya mafanikio hayo. “Kwanza nipongeze waratibu wa tamasha lenyewe, hii ni moja ya sehemu muhimu katika kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo nchini.

“Kama kiongozi serikalini, hakika nimeguswa kwa kiasi kikubwa kuona wapo baadhi ya watu wanajali vipawa vya Watanzania wenzao. Naamini zipo sekta mbalimbali zitanufaika na tamasha hilo, ‘especially’ uwepo wa Azam TV.

“Kuhusu tuzo yangu, binafsi mimi ni mtu wa mazoezi. Nimejiwekea ratiba ya kufanya mazoezi kila siku kukimbia zaidi ya kilomita tatu. Nauzunguka Uwanja wa Majimaji (unaotumiwa na timu ya Majimaji) mara tano na kuchukua ‘session’ nyingine ya mazoezi. Ndiyo maana haikuwa shida sana kukimbia.

“Pili sinywi pombe, mambo ya starehe kwangu ‘no’, hivyo pamoja na uzee wangu, miaka 38, nimewachachafya watoto wadogo, najua walikuwa wakinibeza lakini watakuwa wamejifunza kutoka kwangu jinsi ya kujitunza ili uwe na afya bora,” anasema.

Msimu wa tatu wa tamasha hilo limepangwa kuwa kati ya Julai 23 hadi Julai 30 mwaka 2017.

Wanafunzi waibuka na IPADS kutoka JICA kwenye tamasha la majimaji

img_0610 img_0611 img_0668 img_0665 img_0670 img_0691 img_0623 img_0619 img_0574img_0662

SO-MI na Tanzania Mwandi katika kuthamini msingi wa maendeleo mashuleni mkoani Ruvuma, Tamasha la Majimaji tangu kuanzishwa kwake wamekuwa wakiratibu mihadalo kwa shule za sekondari ambapo mwaka huu mwitikio ulikuwa mkubwa zaidi.

Tofauti na mwaka jana ambapo shule tano ndizo zilizoshiriki, mwaka huu zilishiriki jumla ya shule 11, huku pia waratibu wakiboresha zaidi zawadi kwa washindi, kwa kutoa IPad kwa shule tatu zilizofanya vizuri, IPad zenye notice ya masomo yote kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita kama sehemu ya kuwarahishia ufaulu kwenye mitihani yao. Shukrani za kipekee ni kwa Shirika la Maendeleo la Kijapani (JICA) waliotoa sapoti hiyo ya IPad.

Shule ya De Paul iliibuka kidedea ikifuatiwa na St. Agness huku Shule ya Wasichana ya Songea ikishika nafasi ya tatu, ambapo mbali na IPad washindi wote walitunukiwa ngao ya ushindi. Shule ya Kingosera ambayo ilikuwa ikitetea ubingwa wake wa mwanzo, iliambulia patupu safari hii, huku ikikosekeana hata kwenye Tatu Bora licha ya kuanzia hatua ya mtoano moja kwa moja.

Mkurugenzi Mwakilishi wa JICA, Toshio Nagase aliambatana na wajumbe wenzake wa shirika hilo, Jacob Katanga, Kei Umetsu, Zuhura Mwakijinja, walihudhuria mdahalo huo wakiungana na mwanachama wa JATA, wakili Dk. Damas Ndumbaro ambaye ni Mkurugenzi Mwenza wa Asasi ya SO-MI.

Utalii wa ndani

Mbali na burudani ya ngoma za asili zilizokonga nyoyo za wananchi waliohudhuria tamasha hilo, pia kulikuwa na utalii katika vivutio mbalimbali vilivyoko mkoani humo kama vile hifadhi ya mbuga za wanyama ya Luhira, hifadhi ya misitu ya Matogoro (Matogoro Forest Reserve), mradi wa ufugaji wa samaki katika mabwaba ya Ruhila, sehemu zote zipo kilomita chache kutoka Songea Mjini.

Siyo hayo tu, pia washiriki walipata nafasi ya kujionea mfano wa kuigwa kwa wanamke kutokana na mradi mkubwa wa ufuaji umeme eneo la Tulila, lililopo zaidi ya kilomita 50 kutoka Songea Mjini. Huu ni mradi ulioanzishwa na huendeshwa na masista tu wa Kanisa la Mtatifu Benedict. Chochote kile katika mradi huu huendeshwa na wao na katu huwezi kukutana na sura ya kiume hata awe mlinzi!  Wao ndio hukesha wakibadilishana zamu ya kukontroo mitambo, ukarabati wa aina yoyote ile hufanywa na wao tu!

Kwa kweli ilikuwa ni zaidi ya maajabu, hasa kuzingatia ukubwa wa mradi ambao umeme wake ndiyo kutoia huduma mjini Songea nzima pamoja na wilaya jirani. Ni mradi mkubwa sana ambao huwaingizia mamilioni ya fedha kila mwezi kwa huduma yake.

Mbali na mradi wa umeme, pia upande wa pili masista wa kanisha hilohilo lakini wao wakitokea Chipole, waliwashangaza wengi kwa ubunifu wa bidhaa mbalimbali, ambazo kwenye maonyesho ya ujasiriamali zilishika nafasi ya pili. Miongoni mwa bidhaa zao zilizokubalika zaidi ni mvinyo uliyotengenezwa kwa ubora wa hali ya juu na mishumaa na soseji.Siyo hayo tu, washiriki pia walitembelea mradi wa ufugaji samaki katika Mabwawa ya Ruhila na kupata kupewa elimu juu ya ufugaji.

Jakaya Group waibuka vinara kwa mara ya pili.

img_0135

Haikuwa rahisi kupatikana kwa bingwa wa ngoma za asili, kiasi cha kuwalazimu waratibu wa tamasha kutumia siku mbili ili kujidhirisha na aliyestahili kupewa zawadi ya mshindi. Kwanza ni kutokana na wingi wa vikundi, tofauti na msimu wake wa kwanza ambako vilishiriki vikundi tano, safari hii vilichuana vikundi 12 pili ni ushindani wa hali ya juu.

Mazingira haya yalipelekea kutengwa kwa siku mbili, ambapo siku ya kwanza ilikuwa ya mchujo katika mfumo wa makundi ambapo kulikuwa na makundi matatu; Ngoma ya Mganda, Kioda na Ngoma ya Mchanganyiko. Kila kundi lilitoa bingwa kabla ya kukutanishwa siku iliyofuatia.

Kikundi cha Jakaya Sanaa Ngoma ya Lizombe kutoka Lizaboni, kiliibuka bingwa katika fainali ya mabingwa kwa kuviangusha Kilagano Ngoma ya Mganda (wa pili) na Boma Jaribu Ngoma ya Kioda iliyoshika nafasi ya tatu.

Washindi wote walitunukiwa zawadi ya kombe, cheti seti za fulana na fedha taslim, lakini katika kujali zaidi fani ya watu, Asasi ya Somi na Kampuni ya Mwandi Tanzania wakaingia mkataba wa kimasoko na bingwa, Jakaya Sanaa kuwatafutia masoko pamoja na kuwapa ofa ya kurekodi nyimbo zake kwenye kamera za kisasa za Azam TV ambao pia walikuwa bega kwa bega mwanzo mpaka mwisho wa tamasha na baadhi ya matukio yakirushwa mubashara ‘live’ ikiwemo fainali hiyo.

Siyo hilo tu, Somi na washirika wake katika kujali kazi zao, bado walimwaga zawadi kwenye hatua ya mchujo wa kusaka bingwa ambapo kulitolewa zawadi kwa washindi watatu kwa kila kategoria. Kinara alipewa laki tatu, mshindi wa pili laki mbili na laki moja ilikwenda kwa mshindi wa tatu.