Magufuli atikisa Tamasha la Majimaji Selebuka

Na Mwandishi Wetu

KASI ya awamu ya tano chini ya Amri Jeshi Mkuu, Dkt John Pombe Magufuli imezidi kutikisa kila kona ya nchi, huku wananchi wakizidi kummwagia sifa kede kede.

Ndivyo ilivyokuwa kwenye tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka linaloendelea kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, ambako vikundi karibu vyote vya ushiriki jumbe zao zilihusu ubora, ufanisi wa awamu yake ya utawala.

Mashindano hayo ambayo yalidumu kwa siku mbili na fainali kufanyika Jumanne, Julai 25, mwaka huu yalishuhudiwa Kikundi cha Mganda kutoka Luhagala kikiubuka na ushindi na kujinyakulia kombe na kitita cha laki nne.

Aidha kwa kiasi kikubwa kikundi hicho kilibebwa zaidi na ujumbe wa nyimbo zao katika kuisifia serikali ya Tanzania awamu ya tano kama vile inavyopambana na ufisadi, wala rushwa, kutokomeza biashara ya madawa ya kulevya huku wakimalizia na kibonzo cha HAPA KAZI TU

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Kikundi cha Ngoma cha Ruvuma Championi, kinachoundwa na watoto wanahosiwa kutofikisha miaka 18 ambako waliwakonga nyonyo watazamani kwa umahiri wao wa kucheza ngoma za asili. Waliondoka na kombe na fedha taslim laki tatu huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Kikundi cha Ngoma cha Kioda kinachoundwa na kina mama kutoka Luhagala. Walipewa kombe na fedha taslim laki mbili.

Mbali na fainali hizo, pia maonyesho ya ujasiriamali na utalii wa ndani ni baadhi ya shughuli zinazoendelea. Tamasha hilo litahitimishwa Julai 30, mwaka huu kwa mashindano ya mbio za baiskeli 100km kutoka Wilaya ya Mbinga mpaka Songea.

Mbio za walemavu zageuka gumzo kwenye Tamasha la Majimaji Selebuka Mjini Songea.

Na Mwandishi Wetu, Songea

(3)
Mshindi wa pili kwenye mbio za walemavu katika tamasha la Majimaji Selebuka, John Stephano zilizofanyika tarehe 23 Julai 2017 mjini Songea kwenye viwanja vya Majimaji.

Hamasa kwenye tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka inazidi kupaa juu, hii ni kutokana na mwitikio chanya unaozidi kujionesha mwaka hadi mwaka, na mwaka huu mbio za walemavu ‘paralympic’ za 21km ndiyo imekuwa gumzo.

Ushiriki wao umetajwa kama chagizo kubwa la watazamaji kurundikana kwenye Uwanja wa Majimaji ambako hakuna kiingilio huku wengi wakionekana kuwapa hamasa tangu mwanzo wa mbio mpaka wanakabidhiwa tuzo, wengi wakiwapongeza kwa ujasili wao wa kuvuta pumzi kwa kilomita 21.

Katika mchuano huo wa kuwania kitita cha laki nne kwa bingwa, Jumapili Julai 23, kitita hicho kilitwaliwa na Shukuru Halfan aliyetumia muda wa dakika 18:13, nafasi ya pili ikichukuliwa na John Stephano aliyetumia muda wa  1:56:32 na kupewa laki tatu na mshindi wa tatu alikuwa Mathias Jolo kwa muda wa 2:08:39 na kuondoka na laki mbili.

Aidha katika jumla ya orodha ya washiriki wa mbio hizo, Halfan alishika nafasi tisa akiwapiku wengi wasio na ulemavu licha ya yeye akiwa na ulemavu wa mkono mmoja. Stephano ana upungufu wa mikono yote wakati Jolo ni mlemavu wa mguu.

Katika mahojiano maalum, Halfan amesema: “Kuna dhana ya walemavu kutojiamini katika kujaribu jambo, lakini kupitia tamasha hili nawashauri wenzangu wawe na moyo wa uthubutu na kujiamini kama wanaweza kazi yoyote sawa na wasio na ulemavu. Angalia, nimeshika nafasi ya tisa katika jumla ya washiriki 15, jiulize nimewapiku wazima wangapi?”